Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka leo kwa mara nyingine tena amekutana na uongozi wa Madereva wa Pikipiki (Bodaboda na Bajaji )-UMAPIDO katika ukumbi wa Polisi jamii jijini Dodoma, lengo likiwa ni kuwakumbusha madereva hao umuhimu wa kazi yao.
“Kazi ya udereva Bajaji na Bodaboda ni muhimu sana hivyo tuilinde tuitunze. Hatutaki kazi ya bodaboda ionekane kama kazi ya vibaka. Bodaboda Kanyaneni kwenye vijiwe vyenu, heshimu kazi yako, penda kazi yako na nafsi yako”. Amesema Mhe. Mtaka.
“Tunataka watu wa Bodaboda waheshimiwe wawe na benki akaunti, wawe na Bima ya Afya iliyoboreshwa, wawe wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya jamii, na mfuko wa Pensheni. Na wapate mafunzo ya usalama barabarani. Tunataka ifikie kiasi cha kwamba ukitaka dereva mzuri wa bodaboda au bajaji basi watu wajue kwamba madereva Wazuri wanapatikana Dodoma”. Amesisitiza Mtaka.
Mhe. Mtaka amewafahamisha madereva hao kwamba , ili kuboresha huduma na ulinzi wa dereva na abiria, kuna mfumo uliobuniwa na Dkt. Budoya kutoka chuo cha Teknolojia cha Dar Es Salaam (DIT) ambaye ameuwasilisha na kuonyesha namna utakavyofanya kazi.
Dkt.Budoya ambaye ni Mhandhiri wa Chuo cha DIT, ameeleza kwamba mfumo wa bodaboda uliobuniwa una uwezo wa kuchukua taarifa zote za vituo vyote vya bodaboda na bajaji ( Vituo vya Kazi).
Mfumo huo pia una uwezo wa kupata taarifa ya bodaboda mwenyewe na mzunguko wake.
Kupitia Mfumo huo abira anaweza kuchukua taarifa za dereva na dereva anaweza chukua taarifa za abiria. Taarifa za Bodaboda zote zitaingia kwenye mfumo, kutia ndani namba ya pikipiki na taarifa zote za Bima na TRA. Mfumo huo utasaidia kujua madereva wote waliosajiliwa, na unaweza kuunganishwa na TRA, Bima na maeneo mengine kwa mfano benki.Pia mfumo huo utasaidia kujua endapo dereva Bodaboda au bajaji ameshiriki kwenye uhalifu.
Baada ya mawasilisho hayo madereva wa bodaboda na bajaji walitaka kujua hivi vifaa vinapatikana wapi na gharama ya Kifaa na endapo italipiwa kwa mwezi au mwaka? Je kifaa hicho kinafungwa wapi¬? Je Kutakuwa na mfumo wa mawasiliano na taasisi zingine endapo hatari itatokea?
Akijibu Maswali hayo Dkt. Budoya aliwaeleza kuwa mfumo huo upo tayari japo haujaanza kufanya kazi na gharama yake itakuwa kati ta Tsh. 30,000/- hadi Tsh.50,000/- na unalipiwa mara moja tu. Kifaa hicho kinafungwa kwenye pikipi na kitakuwa na uwezo wa kujua njia zote ambazo pikipiki au bajaji zimepita kwa siku hiyo. Mfumo huu unaunganishwa na Taasisi zingine kama Bima, TRA, Polisi na kwingineko. Mfumo huo unaweza kuboreshwa kwa kuweka kitufe ambacho anaweza kubonyeza mara pale anapohisi hali ya hatari na taarifa hiyo kuwafikia wahusika.
Akihitimisha uwasilisho wa kikao hicho Mhe. Mtaka aliwataka Madereava wote wa Bajaji na bodaboda Mkoa wa Dodoma, kuwa tayari kwa ajili ya “Bodaboda Day” inayotarajiwa kufanyika siku ya Jumapili 19/6/2022 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, ambapo itarajiwa kuwa takribani madereva 10,000 watahudhuria kikao hicho.
Kwa maelezo ya Mkuu wa Mkoa, katika kikao hicho Taasisi mbali mbali za fedha, Mifuko ya hifadhi ya Jamii, Wauza Bodaboda, Bima ya Afya watashiriki na kutoa mada mbali mbali. Aidha Mfumo wa bodaboda utaelezwa kwa mapana zaidi.
Aidha Mkoa umeandaa zaidi ya Reflector 15,000 ambazo zitagawiwa kwa madereva Bodaboda na Bajaji. Tukio hilo litaenda sambamba na uhuishaji wa Vituo vya bodaboda na bajaji. “Ni siku yenu baada ya ibada madereva wote wa Bodaboda na bajaji muwepo JK Convention Centre, kwani sauti ya wana bodaboda wa DODOMA inaweza badilisha sauti ya nchi nzima”. Amesema Mtaka. MWISHO
Jengo la Mkapa (Mkapa House) Barabara ya Hospitali ya Mkoa
Anuani ya Posta: 914 DODOMA
Simu: +255 26 232 4343/232
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@dodoma.go.tz
Hakimiliki©2016 GWF . Haki zote zimehifadhiwa.