Mkoa wa Dodoma umekua mwenyeji wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika Kitaifa ambayo yamefanyika katika viwanja vya Nyerere Square huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dorothy Gwajima (Mb).
Akiwasilisha salamu za Mkoa, mwenyeji wa maoenesho hayo ya kitaifa, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka , amesema anayofuraha kubwa kwa Mkoa wake kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo na ataomba kuwa mwenyeji wa maadhimisho mengine zaidi.
Akizungumzia suala la matukio ya kikatili wanayofanyiwa watoto, Mhe. Mtaka amesema: “Viongozi wa Serikali za Mitaa katika Mkoa wangu wanafanya jitihada za kuhakikisha haki za watoto zinalindwa na wazazi tujitahidi kupambana na mmomonyoko wa maadili hasa kwa watoto wetu kwa sasa kwani tukiifumbia macho hali iliyopo sasa, tutakuja kutengeneza kizazi cha chokoraa na ombaomba wazee wa baadae”
Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Bunge walipata nafasi ya kusoma risala waliyoiandaa mbele ya Mgeni rasmi ambapo imeelezea kuwa watoto wamekua wahanga wa matukio ya kikatili yanayoendelea katika jamii na wanaumia kusikia matukio hayo yakiendelea kushika kasi kila uchao na wameitaka Jamii kutoa ushirikiano pindi vinapotokea vitendo hivi. Pia wamewataka wadau wa maendeleo ya Jamii kuendelea kutoa ushirikiano ili kutokomeza vitendo vya kikatili kwa watoto.
Nao wadau wa masuala ya haki za watoto ambao nao walishiriki katika maadhimisho hayo, walitoa pongezi kwa Serikali kwa kuanzishwa kwa miongozo itakayowezesha upatikanaji wa haki za watoto kwa urahisi ambapo miongozo hiyo pia italeta mabadiliko makubwa katika kutokomeza ukatili kwa watoto waliopo ndani na nje ya shule.
Mgeni Rasmi Mhe. Dorothy Gwajima, alipata nafasi ya kuongea katika hafla hiyo ambapo alisema kuwa amesikia kilio cha watoto kutokana na risala yao kwa kusikitishwa na vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa watoto wenzao hivyo ametoa salamu za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ameapa kuwalinda watoto , kwani kupitia Wizara yake tayari kunautungaji wa sheria ikiwemo ile Na. 21 ya mwaka 2019 ambayo imerekebishwa na inaendelea kurekebishwa ili iweze kuwawajibisha zaidi wale wote watakaobainika kutenda ukatili kwa watoto.
Mhe. Gwajima ameongeza kuwa baadhi ya vifungu kwenye sheria vimebadilishwa ikiwemo kile cha adhabu kwa mtu atakayebainika kumpa ujauzito mwanafunzi na kuna vituo 427 vya dawati la Jinsia vimeanzishwa kwa lengo la kuwapa nafasi watoto kwenda kutoa taarifa pindi wanapobaini mtu anatenda au anataka kutenda ukatili kwa mtoto au watoto. Mwisho amewaasa wananchi na kuwataka kila mtu afanye kazi katika eneo lake kulinda haki za watoto.
MWISHO
Jengo la Mkapa (Mkapa House) Barabara ya Hospitali ya Mkoa
Anuani ya Posta: 914 DODOMA
Simu: +255 26 232 4343/232
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@dodoma.go.tz
Hakimiliki©2016 GWF . Haki zote zimehifadhiwa.