Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma - UDOM umeiteua hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma kuanza kutumika kutoa huduma za matibabu kwa Wagonjwa wa Corona.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa chini ya Mwenyekiti wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Mahenge kwa kushirikiana na timu ya wataalamu wa Afya wa Mkoa wa Dodoma na uongozi wa UDOM imefanya ziara ya kukagua hospitali ya Chuo hicho na kujiridhisha kuwa itasaidia kuboresha na kuimarisha utoaji huduma kwa wagonjwa watakaothibitika kuugua Corona.
Katika hatua nyingine, Chuo Kikuu cha Dodoma - UDOM kupitia wataalamu wake, kimeanza kutengeneza Barakoa na Vitakasa mikono (hand sanitizer) kwa lengo la kuongeza nguvu na mchango wa Chuo hiko katika kusaidia kupambana na maambukizi ya Virusi vya homa kali ya mapafu (COVID 19) hapa nchini.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Faustine Bee amemwambia Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge aliyeambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma kuwa, Chuo hicho kitaanza kusambaza vifaa hivyo kwa wingi na kwa gharama nafuu ambayo watu na Taasisi wataimudu.
"Kama chuo tumeona tusaidie katika mapambano haya,tutazalisha barakoa na vitakasa mikono kwa bei nafuu" alisema Mkuu huyo wa chuo.
Jengo la Mkapa (Mkapa House) Barabara ya Hospitali ya Mkoa
Anuani ya Posta: 914 DODOMA
Simu: +255 26 232 4343/232
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@dodoma.go.tz
Hakimiliki©2016 GWF . Haki zote zimehifadhiwa.