Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka, ameyasema hayo leo wakati wa maonesho ya Ufundi na Ubunifu yaliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma, jengo la Mkapa (Mkapa House).
Maonesho hayo ya siku moja yamefanyika katika viwanja hivyo mara baada ya Mkuu wa Mkoa kuzungumza na Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam Prof. Preksedis Ndomba juu ya umuhimu wa kubadilisha dhana ya maonesho kuwa sehemu na fursa ya kujitangaza, kujifunza na kuuza bidhaa/huduma. Ubunifu ni biashara hivyo ni vyema wabunifu wote kujiandikisha na kupata hati miliki ya ubunifu wao.
Akizungumza Mhe. Mtaka ameeleza ndoto zake za kutaka kuona Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma zikifanya kazi kwa ubunifu Mkubwa. “Natamani siku moja niione Dodoma ikiwa ‘Silicon Valley’ ya Tanzania”. Amesisitiza Mtaka.
Ubunifu unaweza kuzalisha ajira, hivyo ningetamani kuona wataalamu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri wakiwa wabunifu katika maeneo mbali mbali ikiwemo kuongeza mapato kupitia visima vya maji, kutatua chang’amoto ya Bodaboda na Bajaji,masuala ya taa za Barabarani na Foleni.
“Tuangalie jinsi ya kufanya ubunifu katika kiwango cha Mkoa na hasa sisi Serikali ambao ni walaji. Hivyo ndio maana leo nikaona ni vyema niwakaribishe Halmashauri Na Taasisi zetu za Mkoa wa Dodoma ili mje kuona Na kujifunza.”
“Ni vyema kwenye ofisi zenu mutoe fursa kwa vijana kupata mafunzo kwa vitendo na tusikwazike endapo wanafunzi wanapoomba kujitolea katika ofisi zetu. Nitafurahi sana kuona,watoto wakijitolea.”Amesisitiza Mtaka.
“Tutakuwa tukitumia Viwanja hivi hivi kufanya maonesho ya Teknolojia ili watu wapate uelewa na hivyo kuboresha utendaji kazi na huduma katika mkoa wetu wa Dodoma. Kwa Vijana wanaomaliza Chuo, Mkurugenzi wa Jiji katika Soko la Ndugai kule juu kuna nafasi hivyo ni vema vile vyumba vilivyo wazi tuwape vijana wetu ambao ni wabunifu, baadae wakianza kuingiza hela basi wataanza kulipa kodi. Chuo kiwaingize vijana wabunifu kwenye ‘incubators’ kisha baade waingie katika soko la ajira aidha kwa kujiajiri au kuajiriwa. Ningependa tufungue kituo cha kuzalisha wabunifu na sio chuo kila mahala.”Amesema Mtaka.
Akizungumzia Changamoto mbalimbali za Mkoa pamoja na Halmashauri zake, ambazo anaamini kwa kiasi kikubwa zinaweza kutatuliwa na Ubunifu. Katibu Tawala Mkoa Dodoma, Dkt.Fatma Mganga amezigawa Changamoto hizo katika makundi manne ikiwemo Shida kubwa ya kupoteza mapato hasa kwenye Halamshauri. Dkt. Mganga ametoa mfano wa Mfumo wa maji, ambapo mteja naenda kuchota maji kwa kutumia kadi ambayo inakatwa moja kwa moja na fedha kuingia benki. Pia ameshauri na kuiomba DIT kuja na mfumo huo huo katika kuuza mifugo ili kuepusha fedha kuwa mkononi mwa watu. Alitaja changamoto ya pili ambayo ni Uwajibikaji wa Watumishi – kwani kusaini mahudhurio wakati wa kuingia na kutoka sio kuwajibika, hivyo ni vyema kuja na mfumo ambao unaandika kila anachofanya mtumishi wakati wa saa za kazi. Huu mfumo utafanya watu wawajibike. Suala la uvujaji wa maji ni chamgamoto nyingine ambapo ni vema system iwepo ya kutambua mabomba yaliyopasuka, kusimamia na kukagua mtandao wa maji. Dkt. Fatma ametaja changamoto nyingine zinazohitaji ubunifu kuwa ni upotevu wa Dawa katika vituo vya afya, pungufu wa Waalimu na mfumo wa kusaidia watoto.
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar Es Salaam Profesa Preksedis Ndomba ameeleza kwamba Taasisi ya Teknolojia, DSM ambayo ipo chini ya DIT ina mifumo ya Tehama ya kupima Hali ya hewa,mifumo ya kupima water quality- ambayo taarifa zake unaweza kuzipata kwenye DASH Board au hata simu, kufuatilia miradi ya barabara, Mfumo wa kuchakata matokeo ya mitihani ya wanafunzi, mfumo wa miradi unaoweza kusaidia kujua aina ya mradi kama ni wa mkakati au mradi wa maendeleo, wahusika wote wa mradi, maendeleo ya mradi, malipo yamepangwa kwa awamu gani, kiasi kilicholipwa na bakaa. Pia ubunifu unaweza kutusaidia kujua changamoto na mafanikio. Kuna mfumo ambao unachukua E- system ya Mkoa wote na hivyo kutoa taarifa za wakulima, wahalifu, taarifa za zima moto n.k, kuanzia operation to victims all operational ya fire na kadhalika. “DIT ni center of Excellence, kwenu Mchina ni Mshindani”. Amesema Prof. Ndomba.
“Pamoja na hayo tuna mashine za kubangulia karanga,mashine za kutengeneza chakula cha samaki, mashine ya kutengeneza spear parts za pikipiki, bajaji na magari,Pamoja na teknolojia ya kuchuja maji ya chumvi.Mifumo yote hii tayari ni ya kibiashara, nasi tunaiuza na kutoa huduma baada ya mauzo.”
Aidha Katika maonesho hayo vijana kutoka kundi linalofadhiliwa na SNV nao walishiriki ambapo kiongozi wao Bw. Anorld Mlay alieleza kwamba kupitia ubunifu unalenga kuendeleza Dodoma ya Kijani tayari wameweza kuzalisha mkaa wa bei nafuu kwa kutumia vifuu na uji wa mhogo. Katika Mkoa wa Morogoro kwa kutumia ubunifu vijawa wenzetu wameweza kuzalisha taulo za kike ambazo hufuliwa na kuvaliwa tena.
Wakuu wa Wilaya za Dodoma nao walipata nafasi ya kuzungumza machache ambapo walielezea uhumimu wa “mifumo kwani imekuwa ikijenga nidhamu na uwajibikaji hata sisi viongozi tupo tayari kujifunza na kuitumia”. Mhe. Gift Msuya Mkuu wa Wilaya Chamwino.
Mwisho.
Jengo la Mkapa (Mkapa House) Barabara ya Hospitali ya Mkoa
Anuani ya Posta: 914 DODOMA
Simu: +255 26 232 4343/232
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@dodoma.go.tz
Hakimiliki©2016 GWF . Haki zote zimehifadhiwa.