Mkuu mpya wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Sitaki Senyamule, leo amefanya makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Anthony Mtaka ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa Wa Njombe.
Akiongoza makabidhiano hayo, Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Dkt. Fatuma Mganga amewapongeza wakuu hao wa mikoa ya Dodoma na Njombe kwa kuaminiwa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan ambae amewapatia Mamlaka ya kusimamia na kuendeleza kipande cha nchi. Aidha Dkt. Mganga amewaeleza watumishi wa mkoa wa Dodoma kuwa madhumuni ya kukutana ni kumpokea Mkuu wetu mpya wa Mkoa Mhe. Senyamule na hatimae kushuhudia makabidhiano ambayo atafanya na mkuu wa Mkoa anayeondoka Mhe. Anthony Mtaka.
Dkt. Mganga amemweleza Mhe.Senyamule juu ya mikakati na shughuli mbalimbali za Mkoa zilizo mbeleni ambazo ni pamoja na maonesho ya nanenane Kanda ya Kati yanayoendelea katika viwanja vya nanenane vya Nzuguni, Chanjo ya Uviko -19,na mbio za mwenge wa uhuru ambapo mwenge huo utapokelewa mkoani Dodoma 16/8/2022 na utakuwepo Mkoani Dodoma hadi 23/8/2022.Sanjali na hayo Dk. Mganga amemfahamisha Mkuu huyo kuwa idadi ya watu katika Mkoa wa Dodoma ni takribani watu 2.7mln hii ni kulingana na sense ya mwaka 2012. Aidha Mkoa wa Dodoma una Wilaya 7, Halmashauri 8 na vijiji 822.
Akizungumza Mhe. Anthony Mtaka,ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, amemshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini na kumpa jukumu la kuongoza Mkoa wa Njombe. Mhe. Mtaka amempongeza Mhe. Senyamule kwa kuaminiwa na Rais kwa mara nyingine tena na kuja kuiongoza Dodoma. “Mwaka 2012 Mimi, Mhe. Senyamule na Mhe. Nawanda ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa tuliteuliwa kuwa Wakuu wa Wilaya, lakini leo wote tumekuwa Wakuu wa Mkoa,hili ni jambo la kumshukuru sana mwenyezi Mungu. Mhe. Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala Dkt. Fatuma Mganga ni mtu mwenye roho nzuri na mchapa kazi, pia una Wakuu wa Wilaya Wachapa kazi sana.Kwenye RS tulijenga timu, kwani Mimi nina amini sana kwenye vijana ambao wameemaliza chuo na kutafuta kazi.Hivyo nimekuwa nikitoa nafasi kwa vijana wengi sana waje kujifunza kazi na kupata mazoezi. Aidha Mhe. Mkuu wa Mkoa Wakati wote vipaumbele vyangu ni viwili tu ambavyo ni elimu na uchumi unaohusu watu. Hivyo kama tulivyofanya kazi kwa ushirikiano kwa kipindi cha mwaka mmoja basi naomba mumpe ushirikiano huo huo Mhe. Rosemary Sitaki Senyamule”.Amesema Mhe. Mtaka
Aidha baada ya maelezo hayo Mhe.Mtaka amemkabidhi nyaraka mbalimbali Mkuu mpya wa Mkoa wa Dodoma,nyaraka hizo zikiwa ni pamoja na mpango Mkakati, Randama ya Mpango na bajeti pamoja na taarifa ya utekelezaji wa Chama Tawala.
Baada ya Makabidhiano hayo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary.S.Senyamule, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini. ‘’Nilijua kuhama nitahama ila sio Dodoma. Baada ya kuteuliwa kuja Dodoma nimekuja kutambua ya kuwa kumbe Dodoma sio Mkoa tu kama ilivyo Geita na mikoa mingine bali ni kwa makao Makuu ya Nchi. Na hivyo natakiwa kutimiza matazamio si ya wanadodoma tu bali ya Watanzania wote.Hivyo hii imani niliyopewa inakuwa na uzito wa aina yake. Pongezi kwa viongozi wote.” Amesema Mhe. Senyamule.
Hongereni viongozi wote wa Mkoa wa Dodoma.Hongereni kwa kuwa na mpango mkakati wa miaka 5.Mhe Mtaka nimekuwa nikijifunza mengi kutoka kwako nami nitaendelea kufanya hivyo.Hongera sana kwa Machinga Module kwani ni mfano wa kuigwa kwa nchi nzima.Watumishi wa Dodoma niwasihi muendelee kufanya kazi vizuri hivyo hivyo kwani huu ni mkoa wa kiitifaki,kufanya kazi kwa bidii na maarifa kutasaidia sana kufikia Dodoma inayotarajiwa na watanzania, Dodoma inayofanana na Makao Makuu ya Nchi. Tufanye Dodoma ambayo Mungu na Watanzania wanaitaka .Mwisho
Jengo la Mkapa (Mkapa House) Barabara ya Hospitali ya Mkoa
Anuani ya Posta: 914 DODOMA
Simu: +255 26 232 4343/232
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@dodoma.go.tz
Hakimiliki©2016 GWF . Haki zote zimehifadhiwa.